Miili ya wanajeshi 10 wa Uganda, waliouawa na wapiganaji wa al-Shabaab, nchini Somalia inasafirishwa nyumbani.
Msemaji wa jeshi, Kanali Paddy Ankunda, amesema shambulio hilo "limebadili mambo" na al-Shabaab wanafaa kutarajia "jibu lifaalo".
Wanajeshi 12 wa Uganda waliuawa kwenye shambulio hilo la Jumanne, kwenye kambi ya wanajeshi wa Muungano wa Afrika (AU) Kusini mwa Somalia.
Al-Shabaab walisema waliua wanajeshi 70 wa AU.
Wanajeshi wa Uganda wamo kwenye kikosi cha wanajeshi 22,000 cha AU, kinachokabiliana na wapiganaji hao nchini Somalia.
Kwenye tamko la kwanza kabisa kutoka kwa jeshi la Uganda kuhusu shambulio hilo, Kanali Ankunda alisema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter: "Hatutalegeza juhudi zetu za kusaidia kurejesha amani Somalia licha ya shambulio hilo." Hakutoa maelezo kuhusu miili ya wanajeshi hao wengine wawili waliouawa.
Ripoti nyingine zinakadiria wanajeshi waliouawa kwenye uvamizi huo katika kambi ya Janale, kilomita 90 Kusini Magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, ni kati ya 20 na 50.
Wakazi wanasema shambulio hilo lilianza kwa shambulio la kujitoa mhanga lililotekelezwa kwa kulipua gari lililotegwa bomu kwenye lango la kambi hiyo, na kisha kukawa na ufyatulianaji wa risasi uliodumu zaidi ya saa moja.
Licha ya kupoteza ngome nyingi kusini na kati mwa Somalia, al-Shabaab wameendelea kushambulia vikosi vya serikali na Muungano wa Afrika pande mbalimbali nchini humo.
Wapiganaji hao pia hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara ya kujitoa mhanga Mogadishu.
Post a Comment Blogger Facebook