0

Magufuli ataja mawaziri

Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Lushoto kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Jitegemee
Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Lushoto kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Jitegemee
Wakati zikiwa zimebaki siku 44 kabla ya kufikiwa kwa siku ya kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameamua kuweka wazi sifa za watu atakaowajumuisha katika baraza lake la mawaziri pindi akichaguliwa kuwa mrithi wa Rais Jakaya Kikwete katika serikali ijayo ya awamu ya tano.
Akizungumza mbele ya umati katika mkutano wake wa kampeni mjini hapa jana, Magufuli alisema sifa mojawapo kubwa ya mtu atakayemteua katika baraza lake la mawaziri ni kutokuwa bingwa wa kutoa visingizio vya hapa na pale katika kuhalalisha ucheleweshaji    wa     huduma kwa wananchi.
Kadhalika, alisema sifa ya pili ya mtu atakayemteua kushika nafasi ya uwaziri katika serikali yake ni kuchapa kazi bila kuchoka katika kushughulikia matatizo ya wananchi, huku akigusia kauli mbiu yake ya “Hapa Kazi Tu”.
Magufuli alitaja sifa ya tatu muhimu kwa waziri atakayemteua kuwa ni anayejali matatizo ya wananchi na hata mvumilia ambaye atatelekeza ofisi na kwenda kwenye shughuli zake binafsi.
Alisema sifa ya nne kwa waziri atayekuwamo katika serikali yake ni kujali muda katika kushughulikia kero za wananchi; kwamba kila tatizo likifikishwa kwake alishughulikie kwa wakati na si kinyume chake.
“Nitaweka aina ya mawaziri ambao wao ni kazi tu… wakipelekewa matatizo ya wananchi wanayatatua kwa wakati na sitaki kusikia visingizio kama mchakato unaendelea wala nini… nataka kazi tu,” alisema Dk. Magufuli na kuamsha shangwe kubwa kutoka kwa wananchi waliofika kwa wingi kumsikiliza.
Katika sifa ya tano, Magufuli alisema kila waziri atakayemteua ni lazima aonyeshe wazi kuwa anayo dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania na mara zote atafanya kazi kwa kujua kuwa kipaumbele kikubwa ni kuwatumikia wananchi waliowachagua.
Magufuli alitaja sifa ya sita muhimu zaidi kwa mawaziri wake ni uadilifu na wasiotiliwa shaka na wananchi watakaokuwa wakiwatumikia, huku wakijua kuwa wengi wao (wananchi) ni watu maskini wanaohitaji huduma zote muhimu za kijamii ili kujikwamua kiuchumi.
“Mimi ni mwenzenu ni maskini na nimeishi maisha hayo ya kupanda bajaji, daladala na hata baiskeli… msifanye makosa (siku ya uchaguzi) na kama kweli mnataka maendeleo, basi nichagueni mimi muone kwasababu najua ubaya wa umasikini, “ alisema Dk. Magufuli.
Alisema atafunga mianya yote ya upotevu wa fedha za umma ili fedha zitakazookolewa zielekezwe katika kutoa huduma za jamii kama kuhakikisha kuwa hospitali, zahanati na vituo vya afya vinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.
MASLAHI YA WATUMISHI
Akihutubia katika Jimbo la Mkinga, Dk. Magufuli alisema akichaguliwa na kuingia Ikulu, ataboresha zaidi maslahi ya watumishi wa umma, hasa walimu na madaktari, ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Nikiwa Rais nitakuwa mtumishi wa Watanzania wote. Uwe CUF wewe ni wangu,  ACT – Wazalendo, Chadema, NCCR – Mageuzi wote nitakuwa mtumishi wenu. Hivyo naombeni kura zenu niweze kuwatumikia katika kuleta maendeleo,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza kuwa katika kampeni zake ameamua kutumia barabara za vumbi na zenye makorongo ili ajue shida za wananchi akiingia madarakani aweze kuzishughulia kwa uhakika.
KUFUTA MISAMAHA YA KODI
Akiwa katika Jimbo la Bumbuli, Dk. Magufuli aliahidi kufuta misamaha ya kodi kwa kampuni kubwa ili fedha zitakazookolewa zitumike kusaidia miradi ya maendeleo kama elimu, afya na barabara.
Alisema anazijua kampuni kubwa ambazo zimekuwa zikinufaika na misamaha ya kodi bila sababu za msingi wakati wananchi wa kawaida wakiteseka kwa kukatwa kodi.
Alisema serikali yake haitakubali hata kidogo kuona mamalishe na wamachinga wakikamatwa kila mara na kuteswa na askari mgambo kwa sababu ya kodi ndogo ndogo wakati kuna kampuni kubwa zinazopata faida kubwa lakini hazilipi kodi.
“Hawa wenye makampuni makubwa nadhani wananisikia… kwa sababu ujanja wao wa kubadilisha majina naujua, wanapewa msamaha wa kodi na kila miaka mitano wanabadili jina ili wapate misamaha. Sasa kwa serikali ya Dk. Magufuli, hayo hayatakuwapo,” alisema Magufuli.
Alisema vilevile kuwa atahakikisha anatengeneza nafasi nyingi za ajira ili vijana wengi wapate ajira na kwamba serikali yake itahakikisha umeme unasambaa katika vijiji vyote ili wananchi wautumie kwa shughuli za maendeleo.
Chanzo: NIPASHE

Post a Comment Blogger

 
Top