0

Magufuli awataja hadharani wasaliti

Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. John Pombe Magufuli akionyesha kadi ya aliyekuwa kada wa Chadema Mafinga Gift Sikauka Mwachang'a aliyerudi CCM kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Wambi
Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. John Pombe Magufuli akionyesha kadi ya aliyekuwa kada wa Chadema Mafinga Gift Sikauka Mwachang’a aliyerudi CCM kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Wambi
Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, jana aligeuka mbogo baada ya kuamua kuwataja hadharani watu wanaohujumu kampeni zake kwa kujifanya mchana wako pamoja na usiku wakigeukia upande wa upinzani.
Akiwahutubia wananchi wa mkoani hapa jana katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Dk. Magufuli, alisema kuna mamluki wanaokihujumu chama hicho katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Magufuli aliwataja hadharani baadhi ya makada hao ambao wamekuwa wakiipigia kampeni CCM mchana na usiku wakiwapigia wapinzani.
“Kuna baadhi ya wana-CCM wanatujuhumu sana, wengine nawajua hata majina yao bahati nzuri huwa sisemi uongo bali ukweli, kuna huyu Gasper mchana tunakuwa naye CCM lakini usiku anaungana na wapinzani,” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Dk. Magufuli ilipokelewa kwa mshangao na baadhi ya wananchi na wanachama waliokusanyika uwanjani hapo, kwa kuwa baadhi ya makada hao walikuwa wameketi jukwaa kuu wakifuatila hotuba yake.
Mwandishi wa habari hizi alimshuhudia meneja kampeni wa mgombea huyo, Abdallah Bulembo, akimfuata Magufuli na kumnong’oneza ghafla Magufuli alibadilisha na kudai msaliti ni Gasper Anthony wala si Gasper Kileo aliyetajwa awali.
Hata hivyo, Magufuli baada ya kumaliza hotuba yake alimfuata kada huyo na kumkumbatia huku akimtuliza na kuendelea na msafara wake.
Kada huyo aliyetajwa kuwa msaliti anadaiwa awali kuwa mpambe wa mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vinavyunda Umoja wa Katiba (Ukawa).
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni, Kileo alisema alimuunga mkono Lowassa akiwa CCM, lakini kwa sasa anamuunga mkono mgombea urais wa chama hicho, Dk. Magufuli na wala kwa kilichotokea hatarajii kukihama chama.
Akiwahutubia mkoani Shinyanga, Magufuli amesema hashangai wananchi kuanza kumwita rais kwasababu hata yeye anajua kuwa ndiye atakayeibuka na ushindi mnono kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema wagombea wengine wa nafasi ya urais ni wasindikizaji tu kama walivyo wapambe wa kwenye harusi.
Akizungumza na wananchi wa vijiji mbalimbali katika jimbo la Solwa na Msalala Mkoa wa Shinyanga akiwa katika siku yake ya pili ya kampeni mkoani hapa.
Dk. Magufuli mara kadhaa alikuta wananchi wakiwa wamezuia njia huku wakiimba rais rais rais wakitaka azungumze nao kuhusu atakachowafanyia wakimchagua.
“Mnasema mimi ni rais, nasubiri kuapishwa si ndiyo? Sawa hata mimi najua ntarudi hapa Solwa nikiwa rais kwasababu ushindi kwangu utakuwa wa kishindo na matatizo yenu kwasababu nayajua ntayamaliza mapema mtakaponichagua ,” alisema Dk.Magufuli.
Akiwa katika jimbo la Msalala, Dk. Magufuli alimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Ezekiel Maige kwamba ni kijana mcchapakazi na mwadilifu ambaye aliondolewa kwenye nafasi ya uwaziri kutokana na majungu.
Alisema Maige alikuwa akipigwa vita na Mbunge mwenzake wa Kahama James Lembeli, ambaye alikuwa akitamani kuteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri.
“Huyu ni kijana mchapakazi na mwadilifu nileteeni huyu maana anatosha kuwaletea maendeleo, ana rekodi nzuri na aliondolewa kwenye nafasi yake ya uwaziri kwa kuchongewa na mwenzake kwa chuki tu,” alisema Dk. Magufuli.
Aidha, aliwataka wananchi hao kuwa makini kuchagua wabunge wachapakazi na waadilifu kwasababu wengine kazi yao ni kwenda bungeni kuchukua posho na kuondoka.
Alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wala rushwa wakubwa kwani wanazungumza bungeni kwa nguvu kana kwamba wana uchungu na matatizo ya wananchi lakini wakitoka pembeni wanahongwa na kukaa kimya.
“Kuna mbunge akisimama kuchangia bungeni unaweza kudhani ana uchungu na matatizo yenu kumbe anatafuta umaarufu tu kwasababu anaonekana kwenye televisheni ila akipewa rushwa anawasaliti, msifanye makosa kama hayo,” alisema Dk. Magufuli.
Chanzo: NIPASHE

Post a Comment Blogger

 
Top