0

Serikali yasaini mkopo bil. 240/- kujenga kiwanda cha matrekta

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya,
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
Serikali imesaini mkataba wa mkopo wa Sh. bilioni 240.56 kutoka Serikali ya Poland ili kujenga kiwanda cha kutengeneza matrekta na kuongeza idadi ya maghala ya  kuhifadhia nafaka nchini.

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alitoa kauli  hiyo alipokuwa akizungumza kwenye hafla fupi ya makubaliano yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kufanikiwa kwa mradi huo kutasaidia kuongeza ajira kwa vijana, kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza idadi ya kuagiza matrekta kutoka nje ya nchi.
Serikali ya Tanzania inashukuru Serikali ya Poland kukubali kutoa mkopo huo ambao utasaidia kuongeza uzalishaji wa chakula katika sekta ya kilimo na kuondoa matumizi ya jembe la mkono,’alisema.
Mkuya alisema baada ya kusaini mkataba huo, wanaendelea kufanya maandalizi ya kupokea vifaa mbalimbali vya mradi ili ujenzi wake uanze mara moja.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, alisema ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza matrekta nchini utasaidia kuongeza idadi ya uzalishaji zana hizo za kulimia.
Alisema mradi huo utasaidia  harakati za kutokomeza umaskini uliosababishwa na kilimo cha  jembe la mkono   ifikapo 2025 kila mkulima atumie trekta.
Aidha, Wasira alisema mkopo huo utasaidia ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka toka tani 240,000 za sasa na kufikia tani 400,000.
‘Naendelea kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Poland, Zofia Szalczyk, kujua lini   utekelezaji wa mkataba utaanza,’ alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo wa Poland, Zofia Szalczyk, alisema serikali yake itaendelea kutoa mkopo kwa Serikali ya Tanzania ili kuendelea kukuza uhusiano.

CHANZO: NIPASHE

Post a Comment Blogger

 
Top