0

Utafiti wazua taharuki, waibua maswali tata

Utafiti wa Twaweza
Utafiti wa Twaweza
Matokeo ya utafiti kuhusu uchaguzi mkuu yaliyompa ushindi wa asilimia 65 mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli dhidi ya asilimia 25 za Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yameibua taharuki kubwa huku baadhi wakiupinga, kuunga mkono na wengine kuibua maswali kadhaa magumu.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, katika tukio lililorushwa moja kwa moja (live) na vituo vya televisheni, Mkurugenzi Mkuu wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema utafiti huo uliobebwa na anuani isemayo ‘Sauti za Wananchi’, umefuata taratibu zote za kiutafiti na kuhusisha watu 1,848 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.
Alisema mbali na Magufuli kushinda kwa asilimia 65 ikiwa uchaguzi mkuu utafanyika leo, vile vile chama chake (CCM) ndicho kinachopendwa zaidi na wananchi kwa kiwango cha asilimia 66, kikifuatiwa na Chadema asilimia 22, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) asilimia 3 na Chama cha Wananchi (CUF) asilimia moja. Ukawa unaomuunga mkono Lowassa kwa nafasi ya urais, ni muunganiko wa vyama vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi.
Eyakuze alisema kati ya wahojiwa 10 katika utafiti huo, wahojiwa sita walisema wanatarajia kumchagua mgombea wa CCM ifikapo siku ya uchaguzi.
Hata hivyo, Eyakuze alitahadharisha kuwa utafiti huo hautabiri matokeo ya uhakika ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu, bali ripoti hiyo imelenga kutoa majibu ya baadhi ya masuala kuhusu uchaguzi na pia ni fursa adimu kwa wananchi kusikika na kuwapatia taswira viongozi juu ya wapigakura wao.
Alisema wakati huu ambao kampeni za uchaguzi mkuu nchini zingali zikiendelea, viongozi wasiokubalika au kuwa na sera zisizo na ufanisi wanaweza kukataliwa na kutoa nafasi kwa watu wengine.
Alisema ripoti hiyo inagusia zaidi masuala ya siasa na wagombea, hususan kuhusiana na masuala yanayochukuliwa na jamii kuwa ni kero kwao. Kati ya wahojiwa 10, sita kati yao walisema kwa asilimia 59 huduma za afya ni tatizo la kwanza huku matatizo mengine makubwa kwao yakiwa ni kupatikana kwa huduma ya maji (asilimia 46) na matatizo ya elimu asilimia 44.
“Kwa mwaka huu, matatizo kuhusiana na huduma za kijamii yamekuwa yakizungumzwa zaidi, yakiongozwa na afya, maji na elimu. Mwaka 2012 hadi 2014, tatizo lililotajwa zaidi lilikuwa umaskini na masuala ya kiuchumi. Hivi sasa suala la kiuchumi limeshuka kutoka asilimia 63 hadi 34,” alisema Eyakuze.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wananchi walisema ahadi wanazotoa wabunge hazitekelezeki kwani asilimia 64 walisema wanafahamu ahadi zilizotelewa katika kampeni zilizopita, lakini ni asilimia nane tu ndiyo walisema kwamba mbunge wao ametekeleza ahadi zake.
Vilevile, ripoti hiyo imeonyesha kuwa asilimia 98 ya wananchi wamejiaandikisha kupiga kura na zaidi ya asilimia 90 wamedhamiria kupiga kura mwaka huu. Hata hivyo, ni asilimia 57 tu ya wananchi hao ndiyo waliotaja kwa usahihi tarehe ya uchaguzi kuwa ni Oktoba 25.
Kadhalika, ripoti hiyo inaonyesha vilevile kuwa Magufuli anaungwa mkono zaidi na wanawake kwa asilimia 68 na wanaume kwa asilimia 62 huku Lowassa akiungwa mkono na wanaume kwa asilimia 28 na wanawake kwa asilimia 22. Wagombea hao wanachuana vilevile katika kuungwa mkono maeneo ya vijijini, Magufuli akionekana kukubalika kwa asilimia 66 na mjini asilimia 61 huku Lowassa akikubalika maeneo ya mjini zaidi kwa asilimia 28 huku vijijini asilimia 24
Ripoti ionaonyesha vilevile kuwa wanaomuunga mkono Lowassa wanaamini kwa asilimia 12 kuwa ataleta mabadiliko, wanaoamini kuwa ni mchapakazi ni asilimia mbili, na wanaoamini kuwa ana sera nzuri ni asilimia tatu. Kwa Magufuli, asilimia saba ndiyo wanaoamini kuwa ataleta mabadiliko, wanaoamini kuwa ni mchapakazi asilimia 26 na sera nzuri asilimia tano.
Taasisi ya Twaweza ndio iliyofanya utafiti huo
Taasisi ya Twaweza ndio iliyofanya utafiti huo
MASWALI MAGUMU
Miongoni mwa maswali yaliyojitokeza kuhusiana na ripoti hiyo ni juu ya kufanana kwake kwa kiasi fulani na ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na msemaji wa timu ya kampeni ya mgombea wa CCM, January Makamba, iliyodai vilevile kuwa Magufuli atashinda kwa asilimia 69.3.
Akijibu swali hilo kutoka kwa mmoja wa wananchi waliohudhuria uwasilishwaji wa ripoti hiyo, Eyakuze alisema kuwa ripoti hiyo haina uhusiano wowote na CCM wala chama chochote cha siasa na kwamba, mbinu zilizotumika katika utafiti wake zinakubalika duniani kote.
Kuhusiana na ufafanuzi juu ya matumizi ya simu katika kuuliza wahojiwa, Eyakuze alisema utafiti huo wa kutumia simu za mkononi katika maeneo 200 ya kuhesabia yaliyochaguliwa kutoka Tanzania Bara ulihusisha kaya 10 zilizochaguliwa kutoka katika orodha ya kaya zote.
Alisema mtu mzima mmoja alichaguliwa kinasibu katika kaya na kupatiwa simu inayotumia nguvu ya jua na kila mwezi wahojiwa walipigiwa simu kuhusu mada mbalimbali.
Eyakuze alisema wananchi waliochaguliwa kuhusika na utafiti huo, walichaguliwa sawa sawa na nasibu ni mbinu ambayo hutumika kukadiria wastani wa mgawanyo wa tabia, mtazamo, au maoni ya wananchi na pia ni mbinu inayokubalika na wanasayansi, wanatakwimu wa jamii na pia Ofisi ya Takwimu za Taifa (NBS), vyuo vikuu, kampuni binafsi za utafiti kama za Synovate, Ipsos, Gallup na Pew Research.
TAHARUKI
Kufuatia utafiti huo, wasomi na wanasiasa mbalimbali walitoa maoni yao yanayopinga kwa hoja mbalimbali huku wengine wakiunga mkono.
Mkurugenzi wa taasisi ya Sikika, Irene Kiria, alisema maoni hayo ya utafiti hayawezi kuchukuliwa kuwa ndiyo hali halisi itakavyokuwa kwa sababu kipindi cha wiki mbili tangu kukamilika kwa utafiti huo na sasa kunaweza kutokea jambo lolote linalobadili misimamo ya watu.
“Wiki mbili zilizopita utafiti ndiyo ulikamilika kwa mujibu wa Twaweza. Sasa inawezekana vipi kutueleza matokeo haya sasa… muda wa wiki mbili ni mkubwa. Hali ya siasa inabadilika na kama utafiti huu ungefanyika leo, huenda wangepata matokeo mengine,” alisema Kiria.
Kuhusu hali halisi ya utafiti, alisema tofauti ya CCM na upinzani imekuwa tofauti zaidi kati ya majibu ya tafiti na muonekano wa watu.
Kuhusu matumizi na aina ya watu waliohojiwa kupata tafiti hizo, alisema wahojiwa walipewa simu na chaji zake, hali ambayo inaonyesha kunaweza kukosekana kwa uhuru wa kupata takwimu sahihi.
“Kitendo hiki cha kuandaliwa kwa wataalamu na kupewa vifaa vya kufanyia utafiti kinaweza kuwafanya wafanya utafiti kuandaa majibu mazuri ya kuwajibu wataalamu,” alisema Kiria.
Alisema wanaweza kuhofia kutoa majibu yasiyowaridhisha wataalam kwa kuhofia kutafutwa na kuulizwa mara baada ya utafiti kubainishwa.
Pia akizungumzia kuhusu hali ukosefu wa huduma za jamii kama maji, umeme, elimu na afya kwa zaidi ya asilimia 60, alisema ni kweli jambo hilo linalingana na uhalisia.
“Kuhusu takwimu walizotoa juu ya uhalisia wa hali ya maisha ya wananchi kuwa hawana huduma muhimu kama, afya, elimu, umeme na maji ni ukweli usiopingika na wanasiasa wanapaswa kutambua suala hilo,” alisema Kiria.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Alphonce Kessy, alisema hawezi kutoa maoni ya utafiti huo ambao alisema haujabainisha aina ya watu waliohojiwa na kupata majibu ya tafiti.
“Siwezi kutoa maoni ya tafiti ambazo bado sijafahamu ni aina gani ya watu waliohojiwa… kwa mfano, waliingia ofisi gani? Na pia kujua kama waliingia kanisani, msikitini, ofisi za CCM au vyama vingine vya siasa kuwahoji hao watu na kupata takwimu walizozitoa,” alisema Kessy.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, msemaji wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba, alisema matokeo yaliyotolewa na Twaweza kuonyesha kuwa chama chake kitashinda ni ya kisayansi na hivyo hayapaswi kubezwa kwa namna yoyote ile.
Alisema walioguswa na matokeo hayo wanatakiwa kuwa na uvumilivu katika kupewa taarifa hiyo hata kama ni mbaya kwao.
“Miezi kadhaa iliyopita Twaweza walifanya utafiti na walitoa matokeo kama hayo mimi nikiwa miongoni mwao wahusika na nilikuwa mbali na aliongoza mgombea mwingine kwanini asingenifanyia upendeleo kama kigezo ni ukaribu wetu?…”alihoji na kuongeza.
“Kama wanaubeza utafiti huo kwamba amechakachua mimi nashauri wamuombe radhi Eyakuze wanamkosea sana, alisema Makamba.
Chanzo: NIPASHE

Post a Comment Blogger

 
Top