0

Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Uteuzi wa wakuu wa wilaya umepokelewa kwa hisia tofauti na wasomi na wanasiasa, ambao wamedai nafasi hiyo imekuwa kama kichaka cha kuwahifadhi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho.
Rais Jakaya Kikwete juzi aliteua wakuu wa wilaya wapya 13 na wengine kuwahamisha katika vituo vyao vya kazi zikiwa zimebakia siku 18 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambao wananchi watatumia demokrasia yao kumchagua Rais mpya, wabunge na madiwani.Miongoni mwa walioteuliwa wamo makada wa CCM ambao walichukua fomu ya kuwania ubunge lakini wakaangushwa kwenye mchakato wa kura za maoni.
Walioangushwa lakini wametueliwa kuwa wakuu wa Wilaya ni Richard Kasesera ambaye anakuwa Mkuu wa wilaya Iringa. Kasesera aliangushwa kwenye kura za maoni katika jimbo la Rungwe Magharibi mkoani Mbeya.
Wengine ni Asumpta Mshama ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe aliyeangushwa Jimbo la Nkenge, mkoani Kagera, Vita Kawawa ambaye aliangushwa katika kura za maoni Jimbo la Namtumbo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mrisho Gambo, ambaye aliangushwa Jimbo la Ilala anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.
Kufuatia uteuzi huo, wasomi na wanasiasa wameuponda wakidai hakukuwa na maana hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwani kufanya hivyo ni kutumia vibaya fedha za umma.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Kitila Mkumbo, alisema CCM imekuwa ikiwazawadia makada wake walioshindwa kwenye kura za maoni za ndani ya chama kwa kuwapa ukuu wa wilaya ili kulipa fadhila.
“Ukuu wa wilaya hauna maana kwa sababu imekuwa ni kama hifadhi ya kuwahifadhi makada wa CCM walioshindwa kwenye kura za maoni za ndani ya chama,” alisema.
Naye Rais Mtendaji wa Chama cha APPT Maendeleo, Peter Kuga Mziray, alisema uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya nne imebakiza siku chache kuondoka madarakani ni  matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Kinachoudhi katika uteuzi huu ni kuteua wale waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM ina maana tuseme hiki cheo cha ukuu wa wilaya ni cha makada wa CCM?,” alihoji.
Mziray alisema kufanyika kwa uteuzi huo katika kipindi hiki ni sawa na kumchagulia Rais mpya ajaye watu wa kufanya nae kazi wakati naye atapanga safu yake ya uongozi na pengine walioteuliwa wanaweza wasiteuliwe  kwenye uongozi wa serikali mpya.
Alisema kuna haja ya kwenda mahakamani kufuta zisiwapo nafasi ya mkuu wa wilaya kwa sababu inaongeza gharama kwa taifa na pia imekosa maana kwa sababu inakuwa kama vya kuwapeleka wanasiasa wa kukilinda chama tawala.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi, alisema kitendo cha Rais Kikwete, kufanya uteuzi huo kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu hakina mantiki bali ni kulipa fadhila ili atakapoondoka madarakani asiwe na maadui.
Wengine walioteuliwa ni Shaaban Athuman Ntanambe ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Thobias  Mwilapwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Ruth Msafiri (Kibondo) na Abdallah Njwayo ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, mkoa wa Lindi. Pia wapo Mohammed Mussa Utaly ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa,  Daudi Yasin (Makete), Honorata Chitanda (Ngara), Christopher Ng’ubyagai, (Mkalama), Hawa Ng’humbi ( Kishapu).
Wakuu wa wilaya waliohamishwa vituo vya kazi ni Fadhili Nkurlu ambaye anatoka Mkalama kwenda wilaya ya Arusha, Wilson Nkambaku amehamishiwa  Arumeru kutoka Kishapu, Francis Miti anahama wilaya ya Hanang kwenda Monduli, Jowika Kasunga anahamia wilaya ya Mufindi kutoka Monduli, Muhingo Rweyemamu kutoka wilaya ya Makete kwenda Morogoro; Hadija Nyembo anahamia wilaya ya Kaliua kutoka Uvinza na Benson Mpyesya anahamia wilaya ya Songea kutoka Kahama.
Chanzo: Amka Tanzania

Post a Comment Blogger

 
Top